Jumanne 28 Julai 2026 - 03:01
Chuo Kikuu cha Al-Zahra mjini Karbala chawa mwenyeji wa Kongamano la Tano la Kimataifa la “Ulingano wa al-Aqsa”

Hawza/ Chuo Kikuu cha Al-Zahra mjini Karbala kilikuwa mwenyeji wa Kongamano la Tano la Kimataifa la “Nidaa al-Aqsa”, lililohudhuriwa na wajumbe na shakhsia kutoka nchi mbalimbali.

Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, Chuo Kikuu cha Al-Zahra mjini Karbala kilikuwa mwenyeji wa Kongamano la Tano la Kimataifa la “Nidaa al-Aqsa”, lililohudhuriwa na wajumbe pamoja na shakhsia kutoka mataifa mbalimbali. Lengo la kongamano hilo lilikuwa kujadili nafasi ya vyombo vya habari na simulizi katika kuiunga mkono kadhia ya Palestina, pamoja na kupata msukumo kutoka katika misingi ya Mapinduzi ya Imam Hussein (as) ili kukabiliana na taarifa potofu na kuielewesha jamii.

Abdul Latif Al-Haj, Mratibu Mkuu wa Kampeni ya Kimataifa ya Haki ya Kurejea Palestina, aliliambia Shirika la Habari la Karbala Alaan kwamba; shughuli hizo zilianza kwa kikao rasmi cha kwanza kilichojumuisha hotuba kutoka kwa taasisi zilizodhamini na kuandaa kongamano hilo pamoja na ujumbe ulioshiriki. Baada ya hapo, kilifanyika kikao kilichobeba anuani “Ushuhuda wa Moja kwa Moja: Simulizi ya Kweli Kutoka Katikati ya Ardhi”, ambapo baadhi ya ndugu wa mashahidi, wafungwa waliokuwa wameachiwa huru, majeruhi na waandishi wa habari wa Kipalestina waliwasilisha ushuhuda wenye nyaraka kuhusu matukio yaliyoshuhudiwa uwanjani. Siku ya kwanza ilihitimishwa kwa ziara ya hiari katika Haram Tukufu ya Amirul Muuminiin Imam Ali (as) mjini Najaf Ashraf.

Aliongeza kuwa; katika siku ya pili, programu hiyo ilijumuisha ziara ya wajumbe mbalimbali katika Haram Tukufu ya Imam Hussein (as), ambapo walipokelewa rasmi na msimamizi wa kisheria wa Haram hiyo. Baada ya hapo walisikiliza hotuba ya kidini, wakaswali Swala ya Adhuhuri kwa jamaa ndani ya Haram Tukufu, na shughuli zikahitimishwa kwa kushiriki katika matembezi ya “Nidaa al-Aqsa” yaliyofanyika katika njia ya mahujaji kati ya Najaf na Karbala.

Aidha, alifafanua kuwa; kikao hicho kinafanyika katika mazingira ya kipekee, licha ya vitisho vya Marekani dhidi ya eneo hili, ikiwa ni uthibitisho wa kuendelea kwa njia hii na kuonesha uhusiano uliopo kati ya dhulma alizo fanyiwa Imam Hussein (as) na yale yanayowakabili watu wanaopambana na dhulma, hususan wakazi wa Ukanda wa Ghaza.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha